Mara zote na siku zote, Yesu ndiye kielelezo na mfano wa namna gani tunapaswa kuishi na kuyaendesha maisha. Yeye anasema, \”JITIENI NIRA YANGU, MKAJIFUNZE KWANGU…\” (Mathayo 11:29). Tunajifunza nini kwa Yesu? Yesu alipokuwa hapa duniani, hakuwa na CAMPAIGN MANAGER, hakuwa na gazeti la kumpigia chapuo au kumtafutia umaarufu. Lakini bado aliwavuta watu maelfu maelfu kila alikokwenda. Si unakumbuka alipowalisha Wanaume 5000, wanawake wengi zaidi na watoto? Hakupiga mbiu kuwakusanya. Hakupiga debe kwa namna yoyote. Bali watu wenyewe walikusanyana wakisema, \”Njoo twende, nimekutana na yule aliyesemwa na manabii, Yesu Mnazareti \”(Yoh 1:41,45). Kilichowavuta watu kwa Yesu si Miujiza. Kilichowavuta kwa Yesu ni kile walichokiona, \”NASI TUKAUONA UTUKUFU, UTUKUFU KAMA WA MWANA PEKEE ATOKAYE KWA BABA, AMEJAA NEEMA NA KWELI\”(Yoh 1:14). Kila walipomwona Yesu, waliona UTUKUFU WA MUNGU. Waliona NEEMA YA MUNGU. Waliona KWELI YA MUNGU. Ndio maana walikuwa radhi kukaa siku 3 mfululizo wakimsikiliza, wakiwa na njaa tumboni lakini shibe na utoshelevu ndani yao. Wakiwa na uchovu na usingizi miilini mwao lakini wakiwa na nguvu tele mioyoni mwao na utukufu wa Mungu ukiwaatamia. Ukiwa na vitu hivi muhimu maishani mwako, hauhitaji KUPIGA DEBE, Marafiki watakuja, watu sahihi watakuja, utafanikiwa na kustawi, utamtumikia Mungu wako na Kuthibitika. Kumbuka, \”HAUHITAJI KUPIGA DEBE\”