NEEMA MBALIMBALI ZA MUNGU
(DIFFERENT GRACES OF GOD)!
Watu wengi wanadhani kuna neema moja ya Mungu. Yaani neema moja ya Mungu ndiyo inayofanya kazi kwenye maeneo yote ya maisha, lakini huu si ukweli!
Kuna neema “mbali mbali” za Mungu ambazo ni muhimu kila mwamini akazijua na kuzitaka kwa bidii kwa BWANA na kulipa gharama inayotakiwa kutembea ndani ya kila moja!
Lengo la somo hili leo ni kukufahamisha mambo kadhaa;
i) Ujue kuwa ziko neema mbali mbali za Mungu
ii) Ujipime uone ni zipi zinafanya kazi maishani mwako na zipi hazifanyi kazi, na ufanye kitu gani ili zifanye kazi.
iii) Ujue kuwa Mungu kwenye ghala lake la neema kuna neema nyingi sana ambazo zinamsubiria mwamini azichukue na zimrahisishie maisha!
Maandiko yanasema;
“Kila mtu kwa kadri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa NEEMA MBALI MBALI ZA MUNGU”
(1Petro 4:10).
Mara ya kwanza kuliona Neno hili la Mungu, nilibaki mdomo wazi…”neema mbali mbali za Mungu…”
Ina maana “kuna neema zaidi ya aina moja?”
“Ina maana mimi nasomaje Biblia nisione hili andiko kwa miaka yote ya wokovu?”
Je nimejikosesha mambo mangapi kwa kudhani kuna aina moja tu ya neema?
Wakati nawaza hivyo, moyoni Roho Mtakatifu alininong’oneza, “Waebrania 4:16)“…
Nilipofungua niligundua kitu cha ajabu sana;
Mungu ANA KITI MAALUM kinachoitwa KITI CHA NEEMA ambacho ndicho kinahusika na utoaji wa neema mbali mbali za Mungu pamoja na rehema zake pia!
Kuanzia wakati huo nilianza kuzitafuta hizo AINA MBALIMBALI ZA NEEMA kwenye Biblia yangu…. Na kwa neema ya Mungu nitakupatia baadhi ya hizo neema mbali mbali za Mungu hapa chini;
1. Neema ya Wokovu
Hii ni neema ya Mungu ambayo ni maalum kwa ajili ya kumuunganisha mtu na Mungu (Waefeso 2:8-9) na pia kumfundisha na kumuwezesha mtu kuukataa ubaya wa kila namna wakati anapoendelea kumngoja Yesu na siku ya kuingia mji wa uzima (Tito 2:11-13)!
Kazi ya neema hii ni kukusaidia kuupata wokovu, na kukusaidia kuutunza hata siku ya Kristo Yesu!
2. Neema ya kuishinda dhambi
“Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamuwi chini ya sheria, BALI CHINI YA NEEMA”
(Warumi 6:14).
“Maana NEEMA YA MUNGU iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; NAYO YATUFUNDISHA KUKATAA UBAYA NA TAMAA ZA KIDUNIA; TUPATE KUISHI KWA KIASI, NA HAKI, NA UTAUWA, KATIKA ULIMWENGU HUU WA SASA…”
(Tito 2:11-12).
Dhambi ina dawa, na dawa yake ni neema ya Mungu!
3. Neema ya kutuepusha na mabaya yanayowapata wengine
“Lakini Nuhu AKAPATA NEEMA machoni pa BWANA…”
(Mwanzo 6:8).
Neema hii ilimponya Nuhu, mkewe, na watoto wake watatu na wake zao wasife miongoni mwa wengine waliokufa katika gharika!
“BWANA asema hivi, WATU WALE WALIOACHWA NA UPANGA, WALIPATA NEEMA JANGWANI…”
(Yeremia 31:2).
Mungu aliwahi kuwaua watu wazima wote wa Israeli Jangwani, isipokuwa Joshua na Kalebu, na wale vijana wadogo pekee. Neema ya Mungu iliwasaidia kuepuka upanga jangwani!
4. Neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji
“Basi na tukikaribie KITI CHA NEEMA kwa ujasiri, ili tupewe rehema, NA KUPATA NEEMA YA KUTUSAIDIA WAKATI WA MAHITAJI…”
(Waebrania 4:16).
“Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu, kwamba kinitoke. Naye akaniambia NEEMA YANGU YAKUTOSHA; Maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu…”
(2Wakorintho 12:8-9).
Kuna neema maalum ya Mungu inayomsaidia mtu wakati wa changamoto na mahitaji!
5. Neema ya kututhibitisha katika wito tuliopewa na Mungu
“Lakini KWA NEEMA YA MUNGU nimekuwa hivi nilivyo; NA NEEMA YAKE ILIYO KWANGU ILIKUWA SI BURE, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, BALI NI NEEMA YA MUNGU PAMOJA NAMI.”
(1Wakorintho 15:10).
“Na Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, NA NEEMA NYINGI IKAWA JUU YAO WOTE”
(Matendo 4:33).
Hakuna mtu anayeweza kupata matokeo makubwa katika eneo lake la wito bila kuwa na neema nyingi ya Mungu juu yake na pamoja naye!
6. Neema ya kupata utajiri
“Maana MMEIJUA NEEMA YA BWANA WETU YESU KRISTO, jinsi alivyokuwa masikini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba NINYI MPATE KUWA MATAJIRI KWA UMASIKINI WAKE…”
(2Wakorintho 8:9).
“Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; Maana Yeye yule ni BWANA WA WOTE, MWENYE UTAJIRI KWA WOTE WAMWITAO…”
(Warumi 10:12).
Kuna Mfumo kwenye Msalaba wa Yesu ambao unabeba utajiri wa mwamini, na umefungwa kwenye furushi la neema!
Jana siku ya sita tumeipitia neema ya kuepushwa na mabaya yanayowapata wengine! kesho siku ya nane mpaka ya kumi nitaendelea kuchambua aina moja moja ya neema, naamini Mungu atayageuza maisha yako kwa namna ya kushangaza!
MAOMBI
ASUBUHI
1. Muombe Mungu akupatie (kama HAUJAOKOKA) na akusaidie kutembea katika neema ya wokovu (kama umeshaokoka).
-Akusaidie kuukataa ubaya wa kila namna
-Akupe ushindi dhidi ya tamaa za kidunia
-Akupe kuishi maisha ya haki (huipende haki ya Mungu), usimame upande wa haki bila kujali utapingwa na wangapi
-Akupe kuishi kwa kiasi (nidhamu ya Kifungu, dhidi ya kila kitu ili usije ingia DHAMBINI)
Andiko: Tito 2:11-13
2. Muombe Mungu akupe neema ya kuishi maisha ya utakatifu
-Omba Dhambi isikutawale, uwe chini ya nguvu ya ushindi iliyo ndani ya neema yake (Warumi 6:14, Warumi 6:1-6).
-Omba Mungu akusaidie kuishi maisha ya UTAUWA (Utakatifu) katika dunia hii ya sasa ambayo imeoza, watu kufanya dhambi imekuwa kitu cha kawaida (Tito 2:11-12).
MCHANA
1. Muombe Mungu akupe neema ya kuepushwa na mabaya kama iliyokuwa juu ya Nuhu na familia yake, na ambayo ni haki ya wenye haki ndani ya Kristo (Mwanzo 6:8, Zaburi 91:7-12).
-Muombe Mungu mabaya yasikupate wewe wala tauni (magonjwa) yasiikaribie hema yako.
-Muombe Mungu wakati wanaanguka kumi elfu kulia na elfu kushoto kwako, wewe ubaki hai na salama pamoja na watu wa nyumba yako.
2. Muombe Mungu akupe neema ya kukusaidia wakati wa mahitaji (Waebrania 4:16).
-Muombe Mungu akupe kila unachokihitaji kwa sababu hakika kipo ndani ya utajiri mkubwa alionao Yesu Kristo (Wafilipi 4:19)
-Muombe Roho Mtakatifu alete suluhu na majibu ya mahitaji yako papo kwa papo kila yanapojitokeza (Yohana 6:1-12).
JIONI
1. Muombe Mungu akupe neema ya kupata utajiri iliyomgharimu Yesu kufanyika masikini ingawa alikuwa tajiri (2Wakorintho 8:9)
-Mkumbushe Bwana ya kuwa Neno lake linasema ya kwamba anao utajiri KWA WOTE WAMWITAO (ukiwemo wewe)- (Warumi 10:12).
2. Muombe Mungu akupe neema ya kukuthibitisha katika lile jambo alilokuumbia ufanye duniani (wito wako).
Maandiko: 1Wakorintho 15:10, Matendo 4:33.
-Wengine ni huduma
•Uchungaji
•Uinjilisti
•Ualimu
•Unabii
•Utume
-Wengine ni biashara na masuala ya uzalishaji fedha
-Wengine ni michezo na burudani
-Wengine ni elimu na ujuzi
-Wengine ni sayansi na teknolojia
-Wengine ni uongozi na siasa
-Wengine ni masuala ya kijamii
-Wengine ni masuala ya habari na vyombo vya habari
KILA MMOJA MUOMBE MUNGU KUKUTHIBITISHA NA KUKUFANYA NYOTA KWENYE JAMBO LAKO, KWA NEEMA HII YA KUTUTHIBITISHA!
NB: TUOMBEE MIMI MCHUNGAJI DICKSON, MKE WANGU MERCY NA FAMILIA NZIMA YA KANISA LA ABC TULILOPEWA KULICHUNGA, NEEMA IONGEZWE KWETU KWA KUMJUA MUNGU NA KRISTO YESU (2Petro 1:2).
Umebarikiwa mno,
Wewe ni mtu mkuu, umebeba majibu ya wengi!
Tukutane kesho siku ya nane.