MFUNGO WA SIKU 10,MASAA 12 -MAY [SIKU YA 09]

UPAKO WA KUWA

(ANOINTING TO BECOME).

UTANGULIZI

Kwenye maisha haya, hatukuja kubahatisha maisha, wala kufanya pata potea!

Mungu ametuumba TUWE MAALUM katika maeneo fulani kwa ajili ya kutusaidia KUTIMIZA KUSUDI LA KUUMBWA KWETU!

Na katika maisha haya wapo watu wengi sana ambao wanaishi maisha yasiyokuwa yao, na kwa sababu hiyo hawana matokeo au hawawezi kuacha alama kwa dunia yao maana MUNGU HAWEZI KUWA NA WEWE MAHALI AMBAKO HAJAKUUMBA NA KUKUWEKA KUWA!

Adamu alipoasi kule bustanini Edeni, Mungu alipokuja kumtembelea, swali lake la kwanza lilikuwa, *”Adamu UKO WAPI?”* akimaanisha kuna mahali (nafasi) alikomuumba kuwa, na akicheki kwenye ulimwengu wa roho, hamuoni pale!

Nini kilikuwa kimetokea?

Adamu alikuwa ametenda dhambi na kuupoteza uwepo wa Mungu (upako) ambao ndio ulimsaidia KUWA VILE MUNGU ALIMUUMBA AWE BUSTANINI EDENI!

Adamu alikuwa bado Edeni lakini HAKUWA VILE MUNGU AMEMUUMBA AWE, kwa sababu UWEPO WA MUNGU (UPAKO) MAALUM WA KUMFANYA KUWA ANAVYOTAKIWA ULIKUWA UMEONDOKA!

Fikiria hii: Ni Adamu huyo huyo ukimuangalia kwa nje, yuko Edeni ile ile, harakati na majukumu yake yanaendelea kama kawaida, lakini Mungu akicheki kwenye ulimwengu wa roho HAMUONI ADAMU kwa sababu dhambi imemuondolea Upako wa kuwa vile Mungu alimuumba awe!

Upako wa kuwa, ulipoondoka juu ya Adamu, alianza kujificha uwepo wa Mungu, na ujasiri wake uliisha.

Upako wa kuwa ulipoondoka juu ya Adamu, alianza kula kwa jasho na kuteseka badala ya Kumilki na kutawala na kutiisha nchi!

Kaini naye alipomuua Habili, na dhambi kuingia maishani mwake, aligeuka kuwa MTU ASIYEKUWA NA KAO DUNIANI.

Alianza kuzurura badala ya kusimama kwa mafanikio katika ukulima wake.

Alianza kuogopa kufa, na alimwambia Mungu kila atakayeniona atataka kuniua, na nitakuwa mtoro na mtu asiyekuwa na kao duniani!

Haya ni baadhi ya matokeo ya kupoteza upako wa kuwa au kutokuwa na upako huu wa kuwa;

i) Utakuwa mbahatishaji duniani maana hauko kwenye eneo ambalo Mungu kakuumbia ung’are.

ii) Utakuwa mzururaji (mtu wa harakati nyingi na mhangaikaji) lakini matokeo madogo mno.

Waswahili wanasema, “juhudi tembo ila matokeo sisimizi!”

iii) Hofu ya kufa inakuwa juu yako.

Hakuna kitu kinampa mtu ujasiri kama kujua kwamba YUKO KWENYE ENEO AMBALO MUNGU ALIMUUMBA KUWA!

Mtu huyu anakuwa na uhakika kuwa usalama wake na uhai wake upo mikononi mwa ALIYEMUWEKA KUWA!

Yeremia aliambiwa na Mungu kwamba, AMEWEKWA KUWA NABII WA MATAIFA (Yeremia 1:4-5), na tokea hapo Mungu mwenyewe ALIMHAKIKISHIA USALAMA NA UHAKIKA WA MAISHA (Yeremia 1:8, 17-19)!

Kila mtu ambaye anahofia kufa au ana hofu ya kufa au anaogopa kuuwawa ni mtu ambaye HAJUI AU HANA UHAKIKA NA NAFASI YAKE ALIYOWEKWA KUWA NA MUNGU!

iv) Unakuwa uchi.

Heshima ya mtu iko kwenye KUWA VILE MUNGU ALIMUUMBA KUWA!

Nje ya mahali (nafasi) ambako Mungu amekuweka kuwa, utagundua uko uchi na THAMANI YAKO ITAKUWA CHINI MNO AU HAIPO KABISA!

Watu ambao wamefanikiwa sana, na wameacha alama ni watu ambao walijua nafasi zao Mungu alizpwaweka kuwa, na baada ya hapo DUNIA ILILAZIMIKA KUWAHESHIMU.

Kila mtu ambaye anaishi maisha ya aibu, yasiyokuwa na thamani, ni mtu ambaye HAIJUI NAFASI YAKE AU HANA UPAKO WA KUWA JAPO ANAIJUA NAFASI YAKE!

Baadhi ya faida za upako wa kuwa;

i) Haubahatishi maisha, kila kitu unakifanya kwa uhakika (Isaya 49:1-7).

ii) Unaelewa nafasi yako, na unawakubali wengine katika nafasi zao, na mnashirikiana kufanya mambo makubwa kwa utukufu wa Mungu badala ya mashindano na vita (Isaya 41:6-7).

iii) Unakuwa na kitu ambacho ni chakula chako, na kinachokupa utoshelevu (Yohana 4:34).

iv) Unakuwa umegundua eneo lako la matumizi, na Mungu anakutakasa na kukufanya chombo safi cha thamani kifaacho kwa matumizi yake (2Timotheo 2:20-21)!

BAADHI YA WATU AMBAO WALIISHI NJE YA WALIYOUMBIWA KUWA, KISHA UPAKO WA KUWA ULIPOACHILIWA JUU YAO, WAKALETA MATOKEO MAKUBWA!

i) Bezaleli mwana wa Huri

Huyu alikuwa mtu wa kawaida, katika jamii ambaye hakuna aliyejua umuhimu wala thamani yake, lakini UPAKO WA KUWA VILE MUNGU ANAMUONA NA ALIMKUSUDIA KUWA ulipokuja juu yake, maisha yake yaligeukia hapo (Kutoka 31:1-11)!

ii) Yoshua mwana wa Nuni

Huyu alikuwa kijana msaidizi wa Musa.

Hakuwahi kuwaza au kufikiri angekaa kwenye nafasi ya Uongozi ya Musa na kuwarithisha Israeli nchi ya maziwa na asali.

Lakini UPAKO WA KUWA ulipokuja juu yake KWA KUWEKEWA MIKONO NA MUSA, alianza kutembea katika HEKIMA YA KIUNGU ambayo ilifanya THAMANI YAKE IPANDE NA ISRAELI WOTE WAMSIKILIZE (Kumbukumbu 34:9)!

iii) Shedraka, Meshaki, Abednego na Danieli

Hawa vijana wanne wa Kiebrania walikuwa watumwa nchini Babeli, na kama tujuavyo mtumwa hana thamani, na wala hana heshima.

Lakini WALIPOJITENGA NA KUMTAFUTA MUNGU, ALIWAPA UPAKO MAALUM katika maarifa, hekima, ujuzi na ufahamu na wakawa MARA KUMI ZAIDI YA WENZAO WOTE na huko huko utumwani WALIKAA KATIKA NYADHIFA ZA JUU ZA UONGOZI (Danieli 1).

iv) Gideoni

Huyu kijana wa Kiebrania alishakata tamaa na maisha, na alikuwa amejiondoa kwenye orodha ya watu wakuu, lakini Mungu aligeuza jumla historia na mwisho wake baada ya kuachilia juu yake UPAKO WA KUWA vile mbinguni wanavyomtazama na kumtarajia (Waamuzi 6:11-18, Waamuzi 7 na Waamuzi 8)!

v) Daudi

Tunajua kijana huyu alikuwa amepoteza kusudi la kuumbwa kwake maana alikuwa kafanywa mchunga kondoo, asiyehesabiwa wala kukumbukwa (kwa umuhimu) katika orodha ya watoto wa nyumba ya Yesse!

Lakini Mungu ALIPOMPAKA MAFUTA MAALUM YA KUWA vile alimuumba awe (1Samweli 16:7,12-13), katika Israeli nzima hakuna Mfalme aliye na utukufu na heshima kama yeye!

vi) Elisha

Huyu alitumia maisha yake kama MKULIMA MDOGO asiyejulikana wala kuheshimiwa katika taifa la Israeli mpaka pale MUNGU ALIPOMPAKA MAFUTA MAALUM yaliyomfanya KUWA NABII MAHALI PA ELIYA MTSHIBI (1Wafalme 19:16-17)!

Ukisoma 2Wafalme sura ya kwanza hadi ya 7 utaona huyu mtu akifanya maajabu baada ya UPAKO WA KUWA, kuwa juu yake!

vi) Bwana Yesu

Kwa miaka 30 ya kwanza ya maisha yake hapa duniani, mbali ya unabii mkubwa juu yake ya kuwa ni Mwokozi na ni Wokovu wa Ulimwengu wote, ALIISHIA KUWA SEREMALA asiyeheshimika wala kuwa na jina miongoni mwa watu wa Nazarethi na Israeli kwa ujumla!

Lakini ALIPOMPOKEA ROHO MTAKATIFU NA KURUDI KATIKA NGUVU ZA ROHO (UPAKO WA KUWA), HABARI ZAKE ZILIENEA KILA MAHARI HADI NJE YA NCHI YAKE (Luka 4:14)!

Akiwa na Upako huu wa kuwa, alithibitika katika wito wake na kuweka msingi ambao KANISA TUMEJENGWA JUU YAKE!

Umewahi kufikiri nini kingetokea kama Yesu asingelipokea upako wa kuwa vile alivyotabiriwa na kuumbwa kuwa?

Ulimwengu mzima ungekuwa umekosa ukombozi.

Ndivyo ilivyo kwa kila mtu ambaye HANA UPAKO WA KUWA…. Haijalishi umetabiriwa na nabii gani, umewekwa wakfu na nani, ama una ahadi zipi toka kwa Mungu… Kama huna upako wa kuwa vile Mungu amekuumba kuwa, UTAISHIA KUWA MWANA WA SEREMALA (ASILI YA UZAO WA MWILI) NA SI MWANA WA MUNGU (AGENDA YA UFALME JUU YAKO)!

Ni muhimu ukumbuke kuwa Mungu aliyegeuza maisha ya wengi kwenye maandiko kwa UPAKO WA KUWA, ndiye huyu tunayemuabudu katika Kristo Yesu.

Kama utaamua kumng’ang’ania anaweza kukupa upako huu utakaokusaidia kuwa vile anavyotaka kuwa na kuthibitika katika eneo hilo!

Maandiko yanasema, “Bali wote waliompokea ALIWAPA UWEZO WA KUWA…” (Yohana 1:12).

Uwezo huu wa kuwa haujaishia kwenye kuwa WANA WA MUNGU tu bali uwezo unaweza kutupa KUWA VILE MUNGU AMETUUMBA TUWE NA TUMZALIE MATUNDA HUKU DUNIANI!

Ndugu yangu, siku ya leo amua kuutafuta UPAKO HUU WA KUWA… Maisha yako hayatabaki yalivyo!

MAOMBI

1. Muombe Mungu akupe neema ya kujitambua wewe ni nani na UMEWEKWA KUWA NANI hapa duniani.

(Yeremia 1:4-5).

2. Omba Upako wa kuwa (uwezo wa kuwa) uachiliwe juu yako na kukuweka panapo nafasi uliyoumbwa kuiishi (Zaburi 118:5).

3. Muombe Mungu akupake mafuta maalum yatakayokuthibitisha katika eneo lako la wito na kusudi (1Wafalme 19:16-17).

4. Muombe Mungu akusaidie usipoteze muda kufanya yale ambayo haukuumbwa kuyafanya, kwa Roho wake akusaidie kugundua yakupasayo kuyafanya (1Wakorintho 2:9-12).

5. Niombe mimi Mchungaji Dickson Cornel Kabigumila, MKE WANGU, kazi ya Mungu ya ABC ya kwamba Bwana Yesu atupake mafuta maalum katika kile alichotuitia (Zaburi 89:20-29).

Tukutane kesho siku ya kumi,

Umebarikiwa,

Umebeba majibu ya dunia yako.

Mwalimu Dickson Cornel Kabigumila,

Mchungaji mwanzilishi,

ABC GLOBAL.

HEKIMA ZA NDOA 4

“Ndoa ni taasisi ambayo unaungana na mtu mwingine ambaye ANAWEZA KUKUTIA MOTO kwenye KULIFUATA NA KULITIMIZA KUSUDI LA MUNGU… Wawili sahihi kila mmoja anakuwa CHUMA

Read More »
Mafundisho
yesunibwana

SEX BEFORE MARRIAGE

#TENDO LA NDOA KABLA YA #NDOA Luka 16:10 [10]Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo

Read More »