MFUNGO WA SIKU 10,MASAA 12 -APRIL [SIKU YA 2 ]

*”IMANI YA KUPOKEA MAJIBU YA MAOMBI (FAITH TO RECEIVE ANSWERS FROM PRAYERS)”

Ukienda kanisani, kwenye mikutano ya injili au semina, na Mtumishi wa Mungu akasema, *”WANAOHITAJI MAOMBI KWA AJILI YA MAMBO YAO WAPITE MBELE”* … Utashangaa watu watakavyopita mbele MBIOMBIO.

Sasa kama hujapata picha vizuri, Jikumbushe nini kinatokea pale Mtumishi wa Mungu MWL MWAKASEGE anapoita watu wanaotaka kuombewa au kuomba kule mbele madhabahuni… Watu hujaa kule mbele na wengine huziba zile njia kwa sababu kule mbele kumejaa!

Umepata picha ya nilichosema??

Sasa pale Mtumishi anaposema “AMEN, TURUDI KWENYE VITI VYETU”… Utashangaa!!

Utashangaa nini? Utashangaa watu wanavyorudi kwa kujivuta na kinyonge… Huwaoni WAKISHANGILIA NA KUMTUKUZA MUNGU KWA KUPOKEA MAJIBU YA KILA WALICHOOMBA!!

Mungu na mimi tulitarajia baada ya maombi kama yale, WATU WANGEANZA KUSHUKURU NA WENGINE KUMSIFU MUNGU KWAKUWA AMEWAPA YOOTE WALIYOMUOMBA, Lakini inakuwa kinyume!

Utagundua kitu hapa: WATU WANA IMANI KWENYE MAOMBI KULIKO MUNGU NA UADILIFU WAKE WA KUJIBU MAOMBI (People believe in prayer than in God and His integrity to answer prayers)!

Ndiyo maana akitoka hapo na akaambiwa na watu “Mme wako cha pombe tumemkuta akiwa kajikojolea kule baa” Utamsikia anasema, “Yaani huyu mwanaume amekuwa msalaba kwangu. Nimeomba kwa ajili yake, nimetoa sadaka. Nimeshirikisha watu lakini AMESHINDIKANA” Wakati dakika kadhaa zilizopita “ALIPITA MBELE KANISANI, KWENYE SEMINA KUOMBEA SUALA LA MME WAKE KUOKOKA NA KUWA MME BORA KAMA MUNGU ALIVYOMUUMBA”

Tunajifunza hapa kuwa watu wana IMANI YA KUOMBA (KUMWENDEA MUNGU) lakini hawana IMANI YA KUPOKELEA MAJIBU YA MAOMBI YAO.

Na hili ni TATIZO KUBWA KWA WENGI WALIOOKOKA.

Utawasikia wanasema “Mtumishi niweke kwenye maombi” au “Mtumishi tukumbuke kwenye maombi yako” Ukiwaambia “Nimeliombea na Mungu ameshafanya” hawakuelewi wala kukubali!

Ni kwa sababu tumejengewa msingi wa kuamini maombi yana nguvu bila kuambiwa umuhimu wa maombi ni majibu yake.

Haijalishi umeomba muda gani, umeombewa na nani, jambo la muhimu si muda wa maombi bali MAJIBU YA MAOMBI.

Tumejengewa msingi wa kuamini kwenye kufunga na kuomba ila hatujaambiwa maana na umuhimu wa kufunga na kuomba ni MAJIBU UTAKAYOPATA NA SI MUDA ULIOFUNGA NA KUOMBA.

Kuomba ni kuzuri na ni muhimu. Kufunga ni kuzuri na ni muhimu. Lakini MAJIBU YA KUFUNGA AU KUOMBA NI YA MUHIMU ZAIDI ya kufunga na kuomba kwenyewe.

Ndiyo maana nataka leo tuzungumzie IMANI HII YA KUPOKELEA MAJIBU YA MAOMBI.

TOFAUTI YA IMANI YA KUOMBEA NA IMANI YA KUPOKELEA.

Tangu tukiwa wadogo, kila mtu ameaminishwa kuwa kuna Mungu.

Haijalishi ni Mungu wa kweli au ni miungu mingine.

Kila mmoja wetu ameaminishwa katika uwepo wa Mungu. Hivyo basi kuna ile hali imejengeka ndani ya watu kuwa Mungu anaweza kutusaidia na akiombwa anatoa majibu.

Ndiyo maana kila dhehebu hapa duniani linaomba.

Waislamu wanaomba. Wahindu wanaomba. Wabudha wanaomba. Waabudu Shetani wanaomba. Wakristo waenda kanisani (wasiookoka na wasioamini wokovu) nao wanaomba. Na Wakristo kwelikweli (Waliookoka) wanaomba.

Hapa issue si maombi, hapa ni kupata majibu ya maombi.

IMANI KATIKA MAOMBI (IMANI YA KUOMBEA) hii inakuja kwa vile mtu anaamini kuwa kuna Mungu.

Na anaamini Mungu ni nguvu kubwa inayoweza kumsaidia kutatua matatizo na changamoto zake.

LAKINI

IMANI YA KUPOKELEA

Ni imani ambayo ni tofauti mno na imani ya kuombea.

Ni imani ambayo mtu anapaswa kuwa nayo kati ya muda wa kuomba hadi muda wa kuona alichoomba katika uhalisia wake.

Hii ni imani ya kung’ang’ania kile “unachotarajia” kuliko kile hasi unachokiona!

Hii ni imani ya kushikilia “ripoti ya Neno la Mungu” kuliko ripoti ya tatizo lako au wanadamu.

Hii ni aina ya imani ambayo INAHAMISHA VITU TOKA ROHONI KUJA MWILINI.

Hakuna MZAZI ANAYEZAA MTOTO bila kuwa na uhakika wa kuzaa. Tofauti na hapo MTOTO ANAFIA TUMBONI.

Ebu tupitie maandiko kadhaa kuhusu IMANI YA KUPOKELEA;

*”…Maana ALISEMA MOYONI MWAKE, NIKILIGUSA PINDO LA VAZI LAKE NITAPONYWA MSIBA HUU…Saa ileile akawa mzima, ukakoma msiba wake…”*

(Marko 5:28-31).

Huyu ni MWANAMKE ALIYETOKWA NA DAMU KWA MIAKA 12.

Hakwenda kwa Yesu kutafuta MAOMBI YA UPONYAJI.

Bali ALIKWENDA KUPOKEA UPONYAJI WAKE.

Kuna wengi walirudi makwao na magonjwa yao na mateso yao, kwa vile tu WALISUBIRI YESU AWAGUSE AU AWAOMBEE… Lakini huyu mwanamke alikwenda KUPOKEA MUUJIZA WAKE… Maana tangu akiwa nyumbani alishajipanga KUPOKEA NA SI KUOMBEWA!!

“Nikiligusa tu pindo la vazi lake, msiba wangu utakoma”

Marko 2:1-5

Utaona habari za ndugu waliomleta ndugu yao ALIYEPOOZA.

Walipofika mahali Yesu alipokuwa walikuta kumejaa hata mlangoni hakuna pa kumpitishia ndugu yao.

Lakini VIZUIZI WALIVYOKUTANA NAVYO havikuwazuia KUPOKEA MUUJIZA WALIOUTARAJIA kwa ajili ya ndugu yao.

Naamini kuna waliokuta pamejaa wakaondoka na kusema watarudi siku nyingine.

Lakini hawa ndugu WALISHAAMUA SIKU HIYO LAZIMA WAPOKEE MUUJIZA WA NDUGU YAO.

Hivyo wakatoboa dari ya nyumba na kumdondosha ndugu yao mbele alipokuwa Yesu.

Biblia inasema, “YESU ALIPOIONA IMANI YAO… akamwambia yule mgonjwa, Umesamehewa dhambi zako na mwisho akamwamuru ainuke na kutembea”

Asikudanganye mtu; IMANI YA KUPOKELEA MIUJIZA NA MAJIBU YA MAOMBI YETU INAONEKANA HATA KWA MANENO NA MATENDO AMBAYO MWOMBAJI ANAYADHIHIRISHA NJE BAADA YA MAOMBI.

-Ukiomba mme; Anza kujiandaa kuwa mke mwema kama Neno linavyomtaja mke mwema.

-Ukiomba uponyaji; Inuka toka kitandani na anza kutembea na acha kujilizaliza na kutaka huruma za watu.

-Ukiomba kazi: Jiandae, jifunze kuhusu miiko na maadili ya kazi, anza kujiandaa na kuweka vitu ambavyo utafanya kwenye hiyo kazi.

Ukiomba mvua: Chukua mwavuli au koti la mvua.

Ukiomba mtoto: Andaa nguo za mjamzito na mtoto na gharama za matunzo.

Yesu alisema:

“Yoyote muyaombayo mkisali, AMININI YA KUWA MNAYAPOKEA, nayo yatakuwa yenu”

(Marko 11:23-24).

Hii ndiyo imani ya kupokelea.

Ukisoma 2Wafalme sura ya 6 na ya 7, utajifunza kwa MTUMISHI WA MFALME ambaye aliambiwa HALI YA UCHUMI WA TAIFA LA ISRAELI itageuka ndani ya masaa 24.

Huyu ndugu HAKUWA NA IMANI YA KUPOKELEA na alimjibu nabii Elisha ya kuwa HILO JAMBO HALIWEZEKANI KUTOKEA IFIKAPO KESHO MUDA KAMA HUO.

Na ilipotokea HAKUFAIDI.

Ukikosa imani ya kupokelea, itakufanya USIYAONE MEMA YANAPOKUJA (Yeremia 17:5-6).

Ukisoma Matendo 3, Utaona habari ya MTU KIWETE TANGU TUMBONI KWA MAMAKE ambaye aliponywa kupitia PETRO NA YOHANA.

Biblia inasema ALIPONYWA KWA IMANI KATIKA JINA LA YESU (Mstari wa 16).

Lakini hatuwezi kupuuza ukweli kwamba Yeye mwenyewe huyu kiwete alichangia kupatikana kwa muujiza wake.

Biblia inasema “ALIWATAZAMA PETRO NA YOHANA AKITARAJIA KUPATA KITU KWAO”

(Mstari wa 5).

“HUWEZI KUPOKEA KWA MUNGU USICHOKITARAJIA”

You can not experience what you don’t expect!

MAMBO YATAKAYOKUSAIDIA KUINUA IMANI YA KUPOKELEA;

1. Jaza Neno la Mungu la kutosha ndani yako kwa maana kiwango cha Neno ulichonacho kinawiana na kiwango chako cha imani.

(Warumi 10:17).

2. Unapopeleka hoja zako kwa Mungu, kama ulivyoamini kwamba yupo na ukaja kumuomba, AMINI PIA KUWA ANATOA NA MAHITAJI YA WALE WAMUOMBAO (Waebrania 11:6).

3. Amini Neno la Mungu ulilosimama nalo maana Mungu si mtu aseme uongo na analiangalia Neno lake alitimize (Hesabu 23:19, Yeremia 1:12).

4. Jizoeze kujikumbusha shuhuda ambazo unazo za matendo makuu ya Mungu kwako binafsi na kwa watu wengine wanaokuzunguka.

Shuhuda zinainua imani ya kupokea (Testimonies are faith boosters).

Shuhuda zinakupa uhakika kuwa mkono wa Mungu uko nawe kukusaidia.

Daudi ALIPOKEA USHINDI DHIDI YA GOLIATI kwa kujikumbusha shuhuda zake mbili za kwanza!

(1Samweli 17:33-37).

5. Tumia MANENO YAKO vizuri.

Una miujiza mdomoni mwako lakini pia una nguvu ya kuharibu miujiza mdomoni mwako.

Kilichomfanya Malaika amfunge mdomo ZEKARIA baba yake Yohana mbatizaji ni kwa sababu huyu mzee alishaanza kupangua/ kuharibu muujiza alioletewa na malaika.

(Luka 1:11-20).

Ukiona huwezi KUKIRI UNACHOTARAJIA ni bora unyamaze kuliko kuharibu na kupeperusha kile malaika wanachokileta kwako baada ya maombi.

Mungu augeuze ulimi wako usitumike kuua miujiza yako, bali utumike kuichochea itokee kwa kukiri Neno na uzima tu huku ukisubiria matokeo kwa ujasiri wote.

Fanyia kazi hili somo, jipambanue ili usije kupeperusha miujiza yako.

WEWE NI MBARIKIWA, NI SHUJAA NA MTU MKUU KWA VIZAZI VINGI VIJAVYO.

TUMIA SIKU HII YA LEO YA PILI YA MFUNGO HUU, KUJIFUNZA KUPITIA SOMO HILI, KUTAFAKARI NA KUIJENGA IMANI YAKO YA KUPOKEA! NA KISHA JIOMBEE SAWA NA ULIVYOELEWA!

NB: ANZA KUANDAA SADAKA YAKO NZURI YA KUAMBATANISHA NA MFUNGO HUU, UTAITOA SIKU YA MWISHO YA MFUNGO, YAANI TAREHE 01/05/2019.

KWA WAOAJI TU

“Ni Hekima Ya Mungu Kumpa Mwanadamu MALIGHAFI [Raw Materials] Ili Yeye [Mwanadamu] Afanye Sehemu Yake KUZIFANYA KUWA BIDHAA HALISI [Products]… Mungu Anakupa MTI Na Ni

Read More »
Mafundisho
yesunibwana

KWA WAOLEWAJI TU

“Kati Ya Mambo Unayopaswa Kuyachunguza Kuhusu Mtu Anayetarajia Kukuoa NI UAMINIFU NA UADILIFU Kwenye MALI NA PESA YA UMMA, KAMPUNI Au WATU WENGINE… Ukiona Huyu

Read More »